Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ali Khamenei leo ameonana na Waziri na maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu pamoja na mabalozi Iran nje ya nchi na kusema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yamekuja na mantiki na siasa mpya katika uhusiano wa kimataifa zilizopewa anwani ya "siasa za kushirikiana dhidi ya mfumo wa kibeberu."
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, jukumu la balozi na mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu nje ya Iran ni kutumia udiplomasia bora, madhubuti na wenye taathira kwa ajili ya kuendeleza siasa za kukabiliana na mfumo wa kibeberu. Amesema sharti la kufikiwa lengo hilo ni kushikamana kwa njia za kimantiki na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na nguzo za sheria za Kiislamu pamoja na kutoona haya ya kuwa na misingi na nguzo hizo.
Akisisitiza kuwa, suala la utekelezaji wa kivitendo siasa za kupambana na mfumo wa kibeberu ni sifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran peke yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kuna pande mbili katika mfumo wa kibeberu ambapo upande mmoja ni wa wafanyaji ubeberu na mwingine ni wa wafanyiwa ubeberu na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza waziwazi tangu mwanzoni kwamba si nchi inayofanya ubeberu na haikubali kufanyiwa ubeberu nchi yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia suala la upya wa siasa za Iran za kupambana na mfumo wa kibeberu duniani na jinsi lilivyokaribishwa na tawala, shakhsia na wasomi mbalimbali katika uga wa uhusiano wa kimataifa na akaongeza kuwa, siasa za kupambana na mfumo wa kibeberu zina misingi na uungaji mkono mkubwa wa kiistratijia, miongoni mwake ni uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa, tofauti na mapinduzi mengineyo, kasi ya harakati kubwa ya wananchi wa Iran haijapungua tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu hadi hivi sasa. Amehoji kwamba, ni nchi gani nyingine duniani ambayo baada ya kupita miaka 31 wananchi wake wameweza kuonyesha uungaji mkono mkubwa kwa utawala wao kama walivyofanya wananchi wa Iran mwaka huu wakati wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu? Amesema, kujitokeza kwa wingi wananchi wa Iran katika maandamano hayo kunaonyesha kuwa si tu uungaji mkono wa wananchi kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran haujapungua bali umeongezeka zaidi na kwamba uungaji mkono huo wa wananchi ni jambo muhimu sana ambalo linashuhudiwa tu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema maendeleo ya kustaajabisha ya kisayansi na kiteknolojia ya vijana wa Kiirani ni nguzo nyingine ya stratijia za siasa za kupambana na mfumo wa kibeberu na kuongeza kuwa, nguzo nyingine kubwa ni kujitokeza wananchi kwa wingi katika chaguzi ambazo ni dhihirisho kubwa la demokrasia ambapo si tu idadi ya wananchi wanaojitokeza katika chaguzi haijapungua, bali imeongezeka sana.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kwamba nguzo nyingine kubwa katika stratijia za siasa za kupambana na mfumo wa kibeberu ni kiwango kikubwa cha ustawi na kazi za maendeleo zilizofanywa na serikali mbalimbali nchini Iran pamoja na ongezeko kubwa la kazi za kijamii nchini na kusisitiza kuwa, nguzo zote hizo za kiistratijia zinatia moyo na zinaandaa uwanja wa kuweza wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufanya mambo yao kwa kujiamini kabisa nje ya nchi na hatimaye kwa kuwategemea wawakilishi hao, ziweze kuendelea siasa mpya za kupambana na mfumo wa kibeberu kwa misingi mitatu ya heshima, hekima na maslahi.
Amesema kutumia nguvu za kidiplomasia kwa ajili ya kuendeleza siasa hizo ni jambo muhimu sana na ameongeza kuwa, nguvu za kidiplomasia hazishindwi na nguvu za kijeshi, kipropaganda na kutumia fedha na hata kuna sehemu nyingi imeshuhudiwa kuwa nguvu za kidiplomasia zinashinda nguvu hizo za kijeshi, kipropaganda na kutumia fedha.
Amesisitiza kuwa inabidi kutumike udiplomasia wenye nguvu, wenye maana na uliosimama juu ya misingi ya kimantiki, busara na moyo wa kujiamini katika kutekeleza siasa za kupambana na ubeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitza kuwa, udiplomasia wenye nguvu na makini kabla ya jambo lolote unahitajia kwanza kuiamini kikamilifu misingi ya kisheria na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na amekumbusha kuwa, katika uga wa kidiplomasia inabidi watu wajiamini kitaifa na kutoona haya katika kushikamana na misingi ya Mapinduzi na nguzo za kidini.
Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa, kushikamana barabara na misingi ya Mapinduzi na sheria ni nguzo muhimu kwa vyombo vya kidiplomasia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, kusimama huko kidete sambamba na kutumia mantiki ni ithibati ya kuwa na nguvu ambazo zitaulazimisha upande unaopinga Mapinduzi ya Kiislamu kuheshimu Mapinduzi hayo na kusalimu amri.
Vile vile amegusia baadhi ya mitazamo isiyokuwa sahihi ya miaka ya huko nyuma kuhusiana na ulazima wa kutumiwa desturi, mbinu na masuala ya kidiplomasia ya Kimagharibi ili kujikurubisha na kujifananisha na Wamagharibi na kuongeza kuwa, watu waliokuwa na fikra hizo potofu walikuwa wakidhani kwamba kwa kuiga mbinu na desturi za kidiplomasia za Magharibi, kungelinyanyua heshima yetu wakati ambapo fikra na desturi za Magharibi zimepitwa na wakati na ni za kipindi cha karne mbili zilizopita, lakini desturi za kidiplomasia na siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni fikra mpya yenye taathira kubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshukuru hatua zilizochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na kupelekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipate mafanikio mbalimbali katika uga wa kidiplomasia na katika suala zima la kukabiliana na changamoto za kimataifa. Ametolea mfano kadhia ya nyuklia na kusema kwamba: "Kwa mfano katika suala la nyuklia na licha ya kuweko wimbi kubwa la uongo, makelele na mashinikizo dhidi ya Mfumo wa Kiislamu, lakini nchi kubwa za kibeberu zimeshindwa kufikia malengo yao katika suala hilo." Ameongeza kuwa, jambo hilo linaonesha kuwa kuna umakini mkubwa katika misingi ya jengo madhubuti la Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tangu awali kabisa ilitangaza kuwa inachotaka ni kuwa na uwezo wa kielimu na kiteknolojia tu katika suala la nyuklia ili iweze kuutumia uwezo huo kudhamini mahitaji yake ya kiraia ikiwa ni pamoja na masuala ya nishati.
Ameongeza kuwa, propaganda na makelele ya mashirika ya baadhi ya nchi za Magharibi zikiwemo Marekani, Uingereza pamoja na Wazayuni kuhusu suala hilo ni uongo mtupu na mashirika hayo yanajua vyema kwamba yanasema uongo na madhara yake upinzani huo yatawarejea wao wenyewe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, pamoja na kuweko mashinikizo yote hayo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata maendeleo makubwa katika upande wa teknolojia ya nyuklia na itaendelea kupiga hatua kadiri itakavyowezekana ili iweze kujitosheleza katika elimu na teknolojia hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amekosoa utendaji wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kuongeza kuwa, baadhi ya hatua na ripoti zinazotolewa na wakala huo zinaonyesha kwamba taasisi hiyo ya kimataifa haiendeshi masuala yake kwa kujitegemea
Amesisitiza kwamba, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haupaswi kukubali uathiriwe na Marekani na baadhi ya nchi kwani vitendo kama hiyo vitaipotezea itibari taasisi hiyo pamoja na Umoja wa Mataifa wenyewe na vitaharibu kabisa heshima na utambulisho wa taasisi hizo za kimataifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kazi ya kimsingi ya Wizara ya Mambo ya Nje ni kutekeleza siasa za kupambana na mfumo wa kibeberu na kuzifanya siasa hizo ziwe na athari katika mahusiano ya kimataifa kwa kutumia udiplomasia wenye madhubuti.
Amesisitiza kwamba inabidi udiplomasia madhubuti utumike zaidi na kila mazungumzo na matamshi yanayotolewa katika uwanja wa kidiplomasia yanapaswa yake makini sana na yatokane na tathmini sahihi.
Ayatullah Khamenei amesisitiza katika sehemu nyingine ya hotuba yake juu ya udharura wa wanadiplomasia wa Iran kutambua vyema fani tata ya udiplomasia na mazungumzo katika miamala yao na ameongeza kuwa, jambo hilo linapaswa kupewe kipaumbele na umuhimu zaidi.
Vile vile amesisitiza kwamba ni jambo muhimu kujenga uhusiano mzuri na wenye athari nzuri na Wairani walioko nje ya nchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Manouchehr Mottaki, alihutubia mwanzoni mwa mkutano huo akisema kwamba ajenda kuu ya mwaka huu ya wawakilishi na mabalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi ni "Mabadiliko katika Uendeshaji wa Masuala ya Kimataifa na Udiplomasia wa Kiadilifu". Anesema kwamba, kuimarisha nafasi ya Iran katika milingano ya kisiasa na kiuchumi ya eneo la Mashariki ya Kati, kudhamini usalama na maslahi ya taifa, kustawisha moyo wa mshikamano wa Kiislamu na kuhami mapambano ya Palestina na Lebanon sambamba na kukabiliana na siasa za kibeberu za madola makubwa, ni miongoni mwa siasa kuu za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ametoa ripoti kuhusu utendaji wa wizara yake katika masuala ya kieneo, jumuiya ya madola, nchi za Asia, Afrika, Amerika ya Latini na Ulaya na kusisitiza kuwa, kumefanyika juhudi mbalimbali katika maeneo yote hayo ili ili kujenga uhusiano unaoegamia kwenye misingi mikuu mitatu ya siasa za Iran katika uga wa kimataifa ambayo ni kulinda heshima, hekima na maslahi.