Ayatullah Khamenei amewapongeza Waislamu wote kwa mnasaba
wa siku ya leo ya kukumbuka tukio la kupewa utume Mtume wetu Muhammad (saw) na akaongeza
kuwa kutokana na kufungua njia za uadilifu, amani, usalama na utulivu, tukio hilo
limetambuliwa kuwa ni rehma ya Mwenyezi Mungu. Ameongeza kuwa njia hizo za
utulivu na amani zinaanzia ndani ya roho ya mwanadamu hadi katika jamii na
dunia nzima na wale wanaotambulishwa na Uislamu kuwa ni wapinzani wa njia hizo
za uongofu ni watu na makundi yanayopinga saada na ufanisi halisi wa mwanadamu.
Huku akisoma aya za Qur'ani Tukufu na kuashiria mwenendo wa
Mtume unaowataka Waislamu kukabiliana na watu wanaopinga saada na ufanisi wa mwanadamu,
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Uislamu umetumia hoja
za wazi katika kuwalingania wanadamu wote maisha ya saada na ufanisi chini ya
kivuli cha amani, uadilifu na usalama, na wakati huo huo umetoa amri ya
kukabiliana vilivyo na watu wanaoweka vizuizi katika njia hiyo."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, katika kipindi
chote cha historia wapinzani wa njia yenye nuru ya saada na ufanisi wa
mwanadamu wamekuwa wakianzisha vita mbalimbali si kwa ajili ya kueneza uadilifu
na amani bali kwa shabaha ya kupanua mamlaka yao, kueneza dhulma na kuvuruga amani
na utulivu wa wanadamu. Ameongeza kwamba hii leo pia madola makubwa ya kibeberu
yanadumisha njia hiyo hiyo ya kijahilia lakini kwa kutumia teknolojia na silaha
za kisasa zikiwemo za nyuklia.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa silaha za madola makubwa ya
kibeberu na gharama kubwa zinazotumiwa kununulia silaha hizo ni miongoni mwa
masuala yanayosikitisha ya dunia ya sasa. Amesema kuwa maadamu madola makubwa
yanaendelea kuongoza masuala ya dunia, basi vita, ukosefu wa amani na dhulma
vitaendelea kushuhudiwa.
Akibainisha kuwa katika kipindi chote cha miaka 45 ya baada
ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia hadi mwaka 1990 kumekuwepo vita dunia
isipokua katika kipindi cha wiki tatu tu, Ayatullah Khamenei amesema vita hivyo
vinaanzishwa na nchi zinazoshika nafasi za kwanza katika kutengeneza silaha kwa
wingi duniani na zinataka kupata faida kutokana na kuuza zana za kijeshi.
Amesisitiza kuwa madai ya Marekani kwamba inaanzisha vita kwa ajili ya
kuimarisha amani na uadilifu ni urongo mtupu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria
takwimu rasmi za gharama za kununulia silaha za Marekani ambazo zimefikia dola
bilioni 600 katika mwaka uliopita na akasema: "Zana hizo za kivita
zinatumiwa kwa shabaha ya kulikandamiza taifa la Waislamu wa Afghanistan,
kulidhibiti zaidi taifa la Iraq na kuusaidia utawala habithi wa Kizayuni wa
Israel kwa ajili ya kuendeleza ghasia na machauko katika eneo la Mashariki ya
Kati.
Amesema inasikitisha kwamba mfumo huo wa kidhalimu na
kijahili ndio unaotawala dunia na maisha ya watu lakini kwa kuwa mwenendo huo
ni kinyume na kanuni za Mwenyezi Mungu katika maumbile na kinyume na haki
hapana budi utatoweka na dalili za kuangamia kwake zimeanza kudhihiri.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria mabadiliko ya hali ya
dunia ya sasa na mwamko unaoshika kasi zaidi wa ulimwengu wa Kiislamu na
akasema: "Moja ya sababu za kuanza kutoweka madola ya kibeberu ni mwamko
wa Kiislamu wa Waislamu ambao umeyafanya madola hayo yapoteze nguzu na uwezo
wao; suala ambalo linathibitishwa na hali ya sasa ya Marekani ikilinganishwa na
miaka ya huko nyuma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu
ya udharura wa kuimarishwa zaidi umoja na mshikamano kati ya Waislamu na akasema:
"Wapinzani wa njia ya tauhidi na ufanisi wa mwanadamu wanahisi hatari kubwa
mahala popote panapokuwa na mwamko zaidi wa Kiislamu na ni kwa sababu hiyo
ndiyo maana uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu umekithiri zaidi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
ni kinara wa mwamko, umoja na heshima ya mataifa ya Kiislamu. Amesema ni miaka
31 sasa ambapo madola ya kibeberu yanafanya njama dhidi ya mfumo wa Kiislamu
hapa nchini lakini licha ya uadui huo Jamhuri ya Kiislamu imepata nguvu kubwa
na kuwa imara zaidi kuliko huko nyuma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa
mwenendo huo utaendelea na kwamba ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni kutoweka
na kuangamia batili. Ameongeza kuwa kadiri kiwango cha uhasama kinavyoongezeka
ndivyo wananchi katika ulimwengu wa Kiislamu wanavyozinduka zaidi. Amezitaka
serikali na mataifa ya Kiislamu kujiamini zaidi na kutoyaogopa madola ya
kibeberu kwani nguvu zao ni bandia, zisizokuwa halisi na zinazotoweka.
Mwanzoni mwa mkutano huo Rais Mahmoud Ahmadinejad
amewapongeza Waislamu kwa mnaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa
utume Nabii Muhammad (saw) na akasema kuwa lengo na hakika na tukio hilo ni
kulingania watu dini inayooana na maumbile halisi ya mwanadamu na kumuokoa kiumbe
huyo. Dakta Ahmadinejad amesema ujumbe wa tukio la kupewa utume Mtume wa Uislamu
ni kuwafanya watu waja wa kweli wa Mola Muumba, neno la tauhidi na kumpwekesha
Mwenyezi Mungu, kueneza uadilifu na kukabiliana na watawala madhalimu na
mashetani, mambo ambayo matokeo yake ni saada na ufanisi wa mwanadamu.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ameashiria woga na wahaka
unaoongezeka kila siku wa madola ya kishetani kutokana na mwamko wa wanadamu na
akasema: "Kama ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyoahidi, ardhi hii watarithi
watu wema, na matunda ya kubaathiwa Mtume wa Uislamu yatadhihiri chini ya
uongozi wa mwanae Imam Mahdi (as)."