Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Ayatullah Ali Khamenei mapema leo siku moja kabla ya maadhimisho ya tarehe tatu
Shaabani inayosadifiana na siku aliyozaliwa Bwana wa Mashahidi Imam Hussein
(as) amehutubia maelfu ya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu
(Sepah) akisema kuwa masuala ya kiroho na kimanawi yanayotawala katika jeshi
hilo ndiyo sababu ya utendaji kazi mzuri wa taasisi hiyo ya wananchi na ya
kimapinduzi katika nyanja mbalimbali na mazingira tofauti ya kipindi cha miongo
mitatu iliyopita. Ayatullah Khamenei amebainisha masuala muhimu ya ndani na ya
kimataifa na akasisitiza kuwa viongozi wote wa nchi hii wanapaswa kutekeleza
majukumu yao mazito katika medani mbalimbali na kujitayarisha kwa ajili ya
kukabiliana na kila jambo kama ilivyokuwa katika kipindi chote cha miaka
thalathini na moja iliyopita. Amesema kuwa hapana shaka taifa kubwa la Iran na
Jamhuri ya Kiislamu itaibuka mshindi katika mpambano huo kama ilivyokuwa huko
nyuma.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameutaja mwezi wa Shaaban kuwa ni mwezi wa dhikri, kuomba na kuijenga upya
nafsi. Ametoa mkono wa baraka na pongezi kwa minasaba ya mwezi huu wa Shaaban
ambayo ni kuzaliwa Imam Hussein, Imam Sajjad na Abul Fadhl al Abbas (as) na akasema
kuwa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni jeshi la wafuasi wa kweli na
wapenzi wa njia ya Mwenyezi Mungu na Maimamu wa njia ya uongofu.
Akifafanua muundo wa kiroho na wa ndani wa
jeshi la Sepah, Ayatullah Khamenei amesema: "Nyoyo zenye hamu kubwa ya
kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu katika medani zote, kusema ukweli na
kuona na kuitambua haki ni mambo matatu yanayounda utambulisho halisi wa jeshi
la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu."
Akiashiria vipengee vya dua tukufu ya mwezi
wa Shaaban, Amirijeshi Mkuu wa majeshi ya Iran amesema kuwa vuguvugu na shauku
kubwa inazikurubisha nyoyo za wanasepah kwa Mwenyezi Mungu na ukweli na ikhlasi
yao katika nia, maneno na matendo inawainua juu na kuwaelekeza kwa Mola Mtukufu,
kama lilivyo neno zuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amekutaja kuona na kutambua haki kuwa ni miongoni mwa nguzo tatu za utambulisho
halisi wa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema sifa hiyo inaliwezesha
jeshi la Sepah kuelewa uhakika wa mambo katika mazingira yote hata katika
machafuko na hali ya kivumbi na ya kutatanisha.
Amirijeshi Mkuu wa majeshi ya Iran ameashiria
historia ya kuasisiwa jeshi la Sepah na kusema kuwa jeshi hilo lilianzia ndani
ya misikiti, shule, vyuo vikuu, nyumba na nyoyo za wananchi wenye imani kubwa.
Ameongeza kuwa hakuna mtu aliyeunda jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu,
bali jeshi hilo lilijitokeza lenyewe kulingana na mahitaji ya zama na lilikidhi
mahitaji ya Mapinduzi ya Kiislamu na taifa mahala popote lilipohitajika.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema
kuwa miongoni mwa sifa kuu za jeshi la Sepah ni kulinda utambulisho wake halisi
na kutenda kazi kwa mujibu wa mahitaji ya zama na wakati. Amesisitiza kuwa
jeshi hilo limeweza kulinda utambulisho wake katika miaka ya awali ya Mapinduzi
ya Kiislamu, katika kupambana na maadui wa Mapinduzi kwenye mitaa ya Tehran,
katika masuala ya mikoa ya mpakani, katika kipindi cha vita vya miaka 8 ya
kujitetea kutakatifu na katika nyanja nyingine nyingi, kwenda na wakati na
kutekeleza vyema majukumu yake.
Akiashiria wito wa viongozi wa wakati huo wa
kulitaka jeshi la Sepah kuingia katika medani za ujenzi na ustawi wa nchi baada
ya vita, Ayatullah Khamenei amesema kuwa katika medani hiyo pia Sepah ilichukua
hatua bora zaidi mahala popote ilipoingia, suala ambalo linaonesha kwamba
taasisi hiyo ya wananchi inakwenda ya wakati na kukamilika zaidi kadiri siku
zinavyopita.
Amesema kuwa suala la kuanzishwa taasisi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na jeshi la Sepah na Jihadi ya Ujenzi ni miongoni
mwa ubunifu na kazi kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Ameongeza kuwa
taasisi hiyo ina muundo unaokwenda na wakati sambamba na kulinda thamani na
malengo yake; masuala ambayo yameiepusha na matatizo yanayozikumba taasisi
nyingine kama hiyo.
Amirijeshi Mkuu wa majeshi ya Iran
amesisitiza juu ya udharura wa kulindwa utambulisho halisi wa jeshi la Sepah na
akasema kuwa taasisi hiyo ni mti uliobarikiwa ambao kwa mujibu wa Qur'ani
Tukufu hutoa matunda makhsusi katika kila kipindi na zama. Amesisitiza kuwa
sifa hiyo nzuri inapaswa kudumishwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
amesema kuwa sharti la kuweza kubuni mipango sahihi kwa ajili ya harakati ya kufanikisha
malengo ya Sepah ni kutambua uhakika wa hali ya sasa, kufanya uchunguzi na
kutabiri hali ya baadaye. Ameashiria wajibu na kazi za makamanda wa jeshi hilo
na Sepah kwa ujumla katika medani hiyo na akasema: "Kulinda utambulisho
halisi wa masuala ya kiroho wa Sepah kunaliwezesha jeshi hilo kutambua uhakika
wa mambo na kutabiri matukio ya siku za usoni." Ameongeza kuwa maarifa na
utambuzi huo vinatayarisha uwanja mzuri wa kubuni na kuchukua hatua sahihi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea
kujadili kadhia hiyo kwa kubainisha hali ya sasa hapa nchini na katika nyanja
za kimataifa. Suala la kwanza ambalo Kiongozi Muadhamu ameliashiria ni uimara
wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Ili kuweza kuweka wazi uhakika huo, Ayatullah
Khamenei amefanya ulinganisho baina ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na
mapinduzi ya Ufaransa na awamu zake mbalimbali zinazokinzana kikamilifu katika
miongo yake ya mwanzoni. Amesema: "Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, tofauti
na harakati nyingine za kisiasa na kijamii za karne hii, yangali yanapiga hatua
katika njia iliyowekwa na Uislamu baada ya kupita miaka 31 ya misukosuko mingi na
Imam Khomeini akaweka njia zake za reli; jambo hili muhimu sana ni dalili ya
himaya na msaada wa Mwenyezi Mungu kwa mapinduzi hayo."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameashiria pia matamshi ya viongozi wa Marekani kuhusu juhudi zinazofanywa na
nchi hiyo kwa ajili ya kubadilisha mwenendo wa Iran na akasema kuwa maana
halisi ya matamshi hayo ni njama za kubadili njia ya harakati ya Mapinduzi ya
Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa nyoyo zenye
imani za taifa la Iran ni dhihirisho la kudura za Mwenyezi Mungu. Amesisitiza
kuwa suala lililobakisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu katika njia yake ya
asili ni mapenzi ya taifa la Iran kwa Uislamu ambao umetengeneza ngome kubwa na
isiyopenyeka kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu na nchi hii; na iwapo njia hiyo
itabadilika na Uislamu kutoweka, ngome hiyo pia itasambaratika na kuruhusu
madhalimu wavamizi kuingia nchini Iran.
Uhakika wa pili ulioashiriwa na Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu hali ya ndani ni maendeleo makubwa ya
taifa hili. Amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, kasi ya maendeleo
na kukua elimu na sayansi nchini Iran imeongezeka mara kadhaa ikilinganishwa na
kiwango cha wastani duniani. Hata hivyo amekumbusha kuwa bado kuna masafa
marefu hadi kufikia daraja za juu za elimu na sayansi ingawa kasi ya sasa haipaswi
kufumbiwa macho.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja
kuiva na kukomaa kisiasa wananchi wa Iran kuwa ni miongoni mwa uhakika usioweza
kupingwa. Ameongeza kuwa wananchi, vijana na mabarobaro wamepata tajiriba na
uzoefu mzuri kutokana na matukio mbalimbali ya kisiasa na wanaelewa vyema mambo
kwa kadiri kwamba hata pale wanaposhawishika katika suala fulani la kutatanisha
hubadilisha mwelekeo haraka na kurejea baada ya kutambua ukweli wa mambo.
Amesisitiza kuwa ukweli huo umeshuhudiwa vyema katika fitina za baada ya
uchaguzi wa Rais wa mwaka jana.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwapo dini
katika maisha ya vijana hapa nchini ni uhakika mwingine muhimu mno. Amesema kuwa
mahudhurio makubwa ya vijana katika ibada ya itikafu, swala za jamaa katika
vyuo vikuu na maeneo mengine na kushiriki kwao katika vikao vya kidini ni ithibati
ya ukweli huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
pia ameashiria suala la kuenea fikra za Mapinduzi ya Kiislamu ulimwenguni.
Amesema kuwa maana halisi ya kupeleka nje Mapinduzi ya Kiislamu ni kupeleka nje
marashi na harufu nzuri ya fikra na malengo ya mapinduzi hayo. Ameashiria pia
jinsi watu katika nchi mbalimbali wanavyowapokea kwa shangwe na furaha kubwa viongozi
wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na akasema: "Harufu nzuri ya marashi ya
Mapinduzi ya Kiislamu imezitia nishati kubwa nyoyo za mataifa mbalimbali, na
huu ni ukweli ambao hauwezi kukanushwa."
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia harakati inayoendelea
ya kambi ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameashiria njama zisizosimama
lakini zilizofeli za utawala ghasibu wa Israel na Marekani kwa ajili ya
kukabiliana na harakati kubwa ya taifa la Kiislamu la Iran na akasema:
"Mapinduzi ya Kiislamu yameiondoa Iran adhimu na yenye nafasi ya
kistratijia na maslahi mengi katika makucha ya Marekani na kukunjua jamvi la
udhalili kwa ajili ya madhalimu wa kimataifa; kwa msingi huo madhalimu hao
wamekuwa wakifanya uadui na njama katika miaka yote iliyopita dhidi ya taifa la
Iran."
Ayatullah Khamenei ameifananisha Marekani na
dhalimu mbabe anayewapokonya watu mali zao katika upeo wa kimataifa lakini hali
yake inakuwa mbaya siku baada ya siku. Amesema baadhi ya wanatoa hongo kwa dhalimu
huyo wa kimataifa kwa ajili ya kulinda biashara zao na wengine wenye nguvu
kiasi wamekuwa wanafunzi wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kutokana na kuchelea
kukabiliana naye. Amesema baadhi ya wengine wanasimama kukabiliana na dhalimu
huyo na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika
mapambano hayo kutokana na kusimama kidete kwa wananchi na viongozi wake.
Akiendelea kufafanua mwenendo unaokuwa kwa
kasi wa kuichukia Marekani kati ya mataifa mbalimbali duniani, Ayatullah
Khamenei ameashiria madai ya nchi hiyo baada ya kusambaratika Urusi ya zamani
na kambi ya Mashariki na akasema wakati huo serikali ya Marekani ilitoa fikra
na mfumo mpya wa kimataifa chini ya uongozi wa White House lakini hii leo
viongozi wa nchi hiyo wanakabiliwa na maandamano na upinzani unaozidi kila siku
wa watu katika pembe mbalimbali za dunia, na chuki na uadui huo wa watu dhidi
ya Marekani haupungui licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi wa
Washington.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria
pia kufeli kwa siasa za Marekani huko Iraq, Afghanistan, Lebanon na Palestina
na akasema: "Licha ya madai yake yote, Marekani na utawala wa Kizayuni wa
Israel zimeshindwa kuiondoa madarakani serikali ya harakati ya Hamas katika
Ukanda wa Gaza na huu ni ushahidi wa ukweli usiweza kupingika nao ni udhaifu wa
nchi hiyo."
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia azimio la
kuiwekea vikwazo Iran lililopasishwa na Baraza la Usalama na vitisho vya mara
kwa mara vya kuishambulia kijeshi Jamhuri ya Kiislamu. Amesema: "Wanatoa
matamshi ya kututaka tufikirie kwamba nyuma ya vitisho hivyo kuna hatari kubwa.
Hata hivyo tunawajibika kujitayarisha kwa hali yoyote ile kwa ajili ya kulinda
Mapinduzi ya Kiislamu na taifa azizi na lenye fahari la Iran, sawa vitisho
hivyo viwe vya kweli au makelele matupu."
Kuhusu kadhia hiyo, Ayatullah Khamenei
amesema kuwa njama nyingi zinazofanywa na Marekani ni za kisiasa na akaongeza
kuwa katika fitina za mwaka jana Wamarekani waliingia katika medani haraka mno
na kuwaunga mkono waziwazi viongozi wa fitina hizo; hata hivyo Mola Muweza,
kuwa macho wananchi na kusimama kidete kwa taifa la Iran kulizima njama na
mipango yao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka
viongozi wote wa masuala ya siasa, uchumi, utamaduni na masuala ya kijamii
kutilia maanani uhakika wa mambo ya ndani ya nje ya nchi na kutaamali utendaji
wa maadui hapa nchini. Amesema hapana shaka kuwa taifa la Iran, Mapinduzi ya
Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu itaibuka mshindi katika mpambano huo kama
ilivyokuwa huko nyuma, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaahidi wamchao kwamba
watapata ushindi wa mwisho na ahadi ya Mola itatimia.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa imani,
ucha-Mungu, amali na matendo mema hutayarisha uwanja mzuri wa kupata ushindi
katika medani za kupambana na maadui wa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza
kuwa mambo hayo yameyalinda Mapinduzi na kuyafanya yashinde mbele ya njama zote
na hali hii itaendelea kuwa hivyo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Amirijeshi Mkuu wa
majeshi ya Iran amesema kuwa propaganda chafu zinazofanywa na maadui na
vibaraka wao wa ndani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni
dalili ya taathira kubwa ya jeshi hilo katika kudumisha harakati imara na ya
fahari ya taifa la Iran. Amewausia pia wanachama wa jeshi hilo kuchunga nafsi
zao na kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu na kazi zo.
Amesema kuwa jeshi la Sepah ni familia moja
kubwa, hai na yenye nishati. Vilevile amesisitiza juu ya udharura wa kuwapo
ushirikiano kati ya sehemu mbalimbali za taasisi hiyo kubwa na akasema hata
askari waliostaafu wa jeshi hilo wanahesabiwa kuwa ni wanachama wake.
Mwanzoni mwa mkutano huo mwakilishi wa Faqihi
Mtawala katika Jeshi la Sepah Hujjatul Islam Walmuslimin Saidi amezungumzia
harakati ya jeshi hilo katika misingi ya sheria na kanuni na akasema taratibu
mpya za jeshi hilo zinatayarishwa.
Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya
Kiislamu Meja Jenerali Ja'fari pia ametoa ripoti fupi kuhusu mkutano wa 19 wa
makamanda na viongozi wa jeshi la Sepah na kusema kuwa miongoni mwa ajenda kuu
za mkutano huo ilikuwa ni pamoja na suala la kujitayarisha kwa hali yoyote,
nafasi na mchango wa jeshi hilo katika mwongo wa nne wa Mapinduzi ya Kiislamu
na njia za kupambana na vita laini.