Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali
Khamenei leo ametoa ujumbe kwa mnasaba wa kutimia siku ya saba tangu kuuawa
shahidi makumi ya wananchi waumini wa mji wa Zahedan huko kusini mashariki mwa
Iran katika milipuko ya kigaidi iliyolenga msikiti mkuu wa mji huo akivitaja
vyombo vya ujasusi vya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza
kuwa ndio wahusika wakuu wa jinai hiyo. Ayatullah Khamenei amesema kuwa moja ya
malengo makuu ya maadui katika kutekeleza shambulio hilo la kigaidi ni kuzusha
hitilafu na fitina za kimadhehebu lakini Jamhuri ya Kiislamu haitaruhusu mikono
ya ubeberu wa kimataifa kufikia lengo lake. Vilevile amevitaka vyombo vyote
husika vya Serikali, Bunge na Mahakama kupambana vilivyo na maadui wa umoja na
usalama wa taifa na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria.
Ujumbe kamili wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ni huu ufuatao:
Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehma Mwenye kurehemu
Siku ya saba tangu kuuawa shahidi kidhulma baadhi ya
wananchi wenzetu waumini na wenye ikhlasi huko Zahedan ambao wameuawa na
wahalifu na magaidi wasokuwa na huruma, imewadia. Katika tukio hilo la umwagaji
damu, mikono ya wahalifu waliopotoka na mawahabi wenye chuki za kimadhebehu
ambao wanasaidiwa na kuchochowe na mashirika ya kijasusi ya kigeni imezitia
simanzi na msiba nyoyo na familia ambazo taa ya mahaba na upendo kwa Watu wa
Nyumba ya Mtume imekuwa ikiwaka ndani yake na nuru ya maarifa na kumpwekesha
Mwenyezi Mungu imezimulikia.
Wahalifu hao wenye chuki za kimadhehebu, vipofu, majahili
na wauaji wamezikabidhi nyoyo zao zilizopotea na nafsi zao zilizojaa giza kwa
madola maovu ambayo yamekuwa yakionesha uadui wao dhidi ya Uislamu mara kwa
mara, na kila mara na mahala zimedhihirisha ufidhuli na chuki yao kwa Waislamu
na kuwahujumu.
Uadui wa madola hayo pia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran unatokana na kupeperushwa bendera ya Uislamu katika nchi hii na wito wake
wa siku zote wa kulingania umoja, nguvu na heshima ya Kiislamu.
Moja ya melengo ya maadui katika tukio hilo la umwagaji
damu na matukio mengine kama hayo ni kuzusha hitilafu kati ya Waislamu. Jamhuri
ya Kiislamu ya Iran ambayo kwa miongo kadhaa imekuwa mtetezi mkubwa zaidi na wa
kuaminika wa Waislamu wanaodhulumiwa huko Gaza, Palestina yote, Afghanistan,
Kashmir na maeneo mengine ya Kiislamu, sasa inalengwa kwa njama hizo chafu za
mashirika ya kijasusi ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Uingereza
ili kwa fikra zao finyu itumbukie katika fitina za kimadhehebu na ugomvi baina
ya Shia na Suni. Maadui hao wameghafilika kwamba Wasuni katika Iran ya Kiislamu
kama walivyo ndugu zao wa Kishia, wamethibitisha mara kwa mara uaminifu wao kwa
utawala mtukufu wa Kiislamu na kusimama kidete kishujaa na kwa imani mbele ya
ubeberu na vibaraka wake kwa ajili ya kuilinda Jamhuri ya Kiislamu na nchi yao
azizi ya Iran.
Kimsingi, kutokea na kukua kwa ugaidi kipofu katika eneo
hili ni matokeo ya siasa zilizojaa uhabithi za Marekani, Uingereza na vibaraka
wao wa kiserikali na usiokuwa wa kiserikali; kwa msingi huo ni wajibu kwa
Waislamu wote kupambana na mwanaharamu huyo najisi ambae ni kilelelezo kikubwa
cha kueneza ufisadi katika nchi na kumpiga vita Mwenyezi Mungu.
Makundi yote ya Ahlusunna nchini Iran na katika nchi jirani
ambayo heshima na hadhi yao ya Kiislamu inashambuliwa kwa siasa hizo habithi
hususan wanazuoni wa kidini, wasomi na wahadhiri wa vyuo vikuu, wana wajibu
mzito zaidi.
Wasomi wa Kishia na Kisuni katika nchi zote za Kiislamu na
Kiarabu wanapaswa kuweka wazi na kubainisha malengo maovu ya maadui katika
kuanzisha na kuimarisha ugaidi wa kimakundi na kuwatahadharisha watu kuhusu
hatari kubwa ya fitina za kimadhehebu ambazo ndio matumaini makubwa ya maadui
wa Uislamu.
Kwa idhini yake Mola Muweza, Jamhuri ya Kiislamu
haitairuhusu mikono ya ubeberu wa kimataifa kuzusha hitilafu kati ya Waislamu
kwa kutumia jina la mawahabi na wengineo kama wao. Vyombo vyote husika vya Serikali,
Bunge na Mahakama vinawajibika kupambana vilivyo na maadui wa umoja na usalama
wa taifa na kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria. Vilevile wananchi wenye imani
wanapaswa kulinda utulivu na kuwa na umaizi na kuwasaidia maafisa husika wa
nchi kutekeleza vyema majukumu yao kwa kujiepusha na harakati yoyote isiyokuwa
ya kimantiki.
Kwa mara nyingine tena ninatuma salamu zangu kwa roho za
mashahidi waliouawa katika shambulizi hilo la umwagaji damu lililofanyika
sambamba na maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bwana wa Mashahi Imam Hussein (as)
na ninatuma salamu za rambirambi kwa familia zao nikizitaka kuwa na subira na
utulivu na kuziombea ujira na malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Vilevile ninamuombea
Mwenyezi Mungu Mtukufu awape shufaa ya haraka watu waliojeruhiwa katika tukio
hilo.
Salamu, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya waja
wake wema.
Sayyid Ali Khamanei
30/Tir 1389 (21 Julai 2010)